Job 37


1 a“Kwa hili moyo wangu unatetemeka,
nao unaruka kutoka mahali pake.

2 bSikiliza! Sikiliza ngurumo ya sauti yake,
sauti ya ngurumo itokayo kinywani mwake.

3 cHuuachilia umeme wake wa radi chini ya mbingu yote
na kuupeleka hata miisho ya dunia.

4 dBaada ya hayo huja sauti ya ngurumo yake;
Mungu hunguruma kwa sauti yake ya fahari.
Wakati sauti yake ingurumapo tena,
huuachilia umeme wake wa radi.

5 eSauti ya Mungu hunguruma kwa namna za ajabu;
yeye hutenda mambo makuu kupita ufahamu wetu.

6 fHuiambia theluji, ‘Anguka juu ya dunia,’
nayo manyunyu ya mvua, ‘Uwe mvua ya nguvu.’

7 gIli wanadamu wote aliowaumba wapate kujua kazi zake,
yeye humzuilia kila mtu shughuli zake.

8 hWanyama hujificha;
hubakia kwenye mapango yao.

9 iDhoruba hutoka katika chumba chake,
baridi hutoka katika upepo uendao kasi.

10 jPumzi ya Mungu hutoa barafu,
eneo kubwa la maji huganda.

11 kHuyasheheneza mawingu kwa maji,
naye husambaza umeme wake wa radi kupitia hayo.

12 lNayo mawingu huzungukazunguka pande zote kwa amri yake,
juu ya uso wa dunia yote,
kufanya lolote ayaamuruyo.

13 mHuleta mawingu ili kuadhibu wanadamu,
au kuinyeshea dunia yake na kuonyesha upendo wake.


14 n“Ayubu, sikiliza hili;
nyamaza na uyafikiri maajabu ya Mungu.

15 oJe, unajua jinsi Mungu anavyoyaongoza mawingu,
na kufanya umeme wake wa radi utoe mwanga?

16 pJe, wajua jinsi mawingu yanavyokaa yakiwa yametulia,
hayo maajabu yake yeye aliye mkamilifu katika maarifa?

17 qWewe unayeshindwa na joto katika nguo zako
wakati nchi imenyamazishwa kimya bila upepo wa kusini,

18 rje, waweza kuungana naye katika kuzitandaza anga,
zilizo ngumu kama kioo cha shaba ya kuyeyushwa?


19 s“Tuambieni yatupasayo kumwambia;
hatuwezi kutayarisha shauri letu kwa sababu ya ujinga wetu.

20 Je, aambiwe kwamba nataka kuongea?
Je, yuko mtu ambaye angeomba kumezwa?

21 tBasi hakuna awezaye kulitazama jua,
jinsi linavyong’aa angani,
upepo ukishafagia mawingu.

22 uKutoka kaskazini yeye huja na fahari kuu;
Mungu huja katika utukufu wa kutisha.

23 vYeye Mwenyezi hatuwezi kumfikia, naye ametukuzwa katika uweza;
katika hukumu zake na haki yake kuu, hataonea.

24 wKwa hiyo, wanadamu mheshimuni,
kwa kuwa yeye hamstahi yeyote anayejidhania kuwa ana hekima.”
Copyright information for SwhKC